Kama rais mstaafu wa Rotary, Paul Harris alisafiri sana katika miaka ya 1920 na 1930, mara nyingi akiwa ameandamana na mke wake, Jean. Wakati wa safari hizi, Harris, aliyependa mazingira, alipanda miti kuashiria nia njema na urafiki.
Katika msimu wa vuli wa 1932, Harris alianza ziara ya wiki tano ya vilabu vya Rotary vya Ulaya na akapanda miti njiani.
“Jumatano asubuhi nilipanda mti wangu wa kwanza wa urafiki katika ardhi ya Ulaya. Ilionekana kwangu kuwa inafaa hasa kwamba ilifanyika Ujerumani — katika jiji lake kuu — Berlin. Upandaji huo ulifanyika katika sports platz ambayo hapo awali ilitumika kwa shughuli za vita, na watu wengi wakiwemo wanachama wa Rotary, maofisa wa jiji, na wengine walihudhuria.”

Paul Harris kwenye upandaji miti huko Bergen, Norway. 1932.

Paul Harris anapanda mti wa urafiki huko Lakeland, Florida, Marekani, mwaka 1942.

Paul Harris anapanda mti mjini Tokyo, mwaka wa 1935.
Tangu wakati huo, Wanarotari wamekuwa wakipanda miti kwa jina la ushirika, urafiki na huduma kwa jamii. Miti hii, inayopatikana duniani kote, imekua na kuwa kumbukumbu za kudumu za maadili ya Rotary.
Baadaye katika ziara yake ya Ulaya, Harris pia alipanda miti nchini Estonia, Norway na Sweden.
Kupanda miti kulikuwa alama ya safari zake, zikiwemo Australia, Brazil, Japan, Mexico na New Zealand. Katika “My Road to Rotary,” Harris alikumbuka, “Kwa ushirikiano wa Wanarotari na serikali za mitaa, nimepanda miti ya urafiki katika bustani na viwanja vya michezo kwenye mabara matano ya dunia na hata kwenye baadhi ya visiwa vikuu vya bahari. Miti yetu ilisimama kama ishara za maelewano ya kimataifa na nia njema.”
Marais wengine wa Rotary pia waliendeleza desturi hiyo. Mwaka 1931-32, aliyekuwa rais wa RI, Sydney W. Pascall, alipanda miti katika maeneo ya vilabu vya Rotary alivyotembelea, ikiripotiwa kwa pendekezo la Paul Harris.
Si miti yote iliyopandwa nje ya Marekani. Mara nyingi akina Harris waliwakaribisha Wanarotari na wageni mashuhuri waliotembelea nyumbani kwao Chicago na walipanda miti pamoja na wageni wao kuadhimisha tukio hilo. Waliiita bustani hiyo Friendship Garden.
Wanarotari wanaendelea kupanda miti kuashiria urafiki wa kudumu na ushirika, kupendezesha bustani na jamii, na kuchangia dunia iliyo ya kijani zaidi.